Wednesday, July 17, 2013

Ujasiriamali

Maana ya Ujasiriamali

Dhana ya ujasiriamali imeelezwa kwa namna tofautitofauti. Baadhi ya watu hufikiri kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara tu. Baadhi wanauangalia ujasiriamali katika muktadha mpana unaohusisha ujuzi na maarifa ya mtu katika kutumia fursa zilizopo. Tranchet na Rienstra, (2009), kwa mfano, wanaelezea dhana ya ujasiriamali kama uwezo binafsi wa mtu wa kubadilisha mawazo na kuwa vitendo. Ujasiriamali unajumuisha ubunifu, kutengeneza kitu kipya na kuwa tayari kukabiliana na ugumu; vilevile kuwa na uwezo wa kupanga na kuendeleza miradi ili kufikia malengo. Dhana hii humsaidia mtu katika maisha yake ya kila siku akiwa nyumbani na katika jamii. Huwafanya waajiriwa kuwa na uelewa kuhusu muktadha wa kazi zao na kuwa katika nafasi nzuri katika kutumia fursa. Pia ujasiriamali hutoa msingi kwa wajasiriamali kujenga shughuli za kijamii au kibiashara. Olomi, (2009) anakubalina na dhana kuwa ujasiriamali kwa ujumla unaweza kuelezewa kama namna ya kufikiri, kutafakari na kutenda inayosababisha utengenezaji, uimarishaji, tambuzi na ufanyaji mpya wa vitu kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu na jamii.

SIFA ZA MJASIRIAMALI 

Baadhi huelezea ujasiriamali kwa kutumia sifa za mjasiriamali. Sifa kubwa za mjasiriamali ni pamoja na :

•Kuwa tayari kupambana na hatari yoyote

•Huchukua uamuzi mapema na hasubiri tatizo likue

•Mvumbuzi

•Mbunifu

•Mwenye kuleta tija

•Mwenye kujitegemea

•Mwenye kutumia fursa zilizopo

•Mwenye kufikia malengo yake

Kwamba, ujasiriamali ni mtazamo katika akili ya mtu katika kutafuta fursa, kuwa tayari kukabiliana na matatizo na kuwa na uwezo wa kutengeneza faida, kwa kuanzisha ama biashara mpya au kuongeza tija katika taasisi. Ujasiriamali hujumuisha shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa na wazo, kutengeneza na kuendesha biashara. Kwamba mjasiriamali ni mtu anayefikiri kwa ubunifu na uvumbuzi akiwa tayari kukabiliana na hatari inayoweza kusababishwa na fursa zilizopo kwa lengo la kuzalisha faida, ajira na ustawi wa kijamii na kiuchumi. Ujasiriamali siyo lazima uhusishe kuanzisha biashara lakini pia kuleta tija au kubadili utamaduni wa shirika au taasisi. Wajasiriamali huanzisha kampuni ambazo huwa injini katika ukuaji wa uchumi na utengenezaji wa utajiri. Kompyuta, simu za mkononi, mashine za kufulia, ATM, kadi za benki na huduma za usafirishaji ni mifano wa mawazo ya ujasiriamali yaliyobadilishwa kuwa bidhaa au huduma.
Ki ukweli ujasiriamali huja kwa kuanza na wazo la kile unachokiona kwamba ni suluhisho la jamii iliyopo, hivyo ujuzi na uzoefu wa  jambo fulani unaweza ukageuza liwe biashara kwa mfano wewe ni kama una fani yeyote yenye kuleta suluhisho au unaweza kufundishwa ujuzi wa kufanya jambo,kutengeneza chochote kigeuze biashara.

MATATIZO HAPA TANZANIA YA UJASIRIAMALI

  • Hapa kwetu tatizo kubwa ni namna ya kupata mitaji ya biashara kwenye tasisi za kifedha.
  • Kodi kubwa kutoka TRA-Habari ndiyo hii unalipa kodi kabla ya kufanya biashara, hapa TRA haitambui kabisa maana hata faida huijui.
  • Wajasiriamali wengi hawana ubunifu katika shughuli zao-uboreshaji wa huduma ama bidhaa kwa maana ya lebo, vifungashio,kauli kwa mteja.
  • Kukosa mpango biashara(BUSINESS PLAN)ambayo ni dira ya njia ya kazi yako.
  • Utunzaji wa hesabu za kazi yako na kutokuwa na kumbukumbu ya mda uliopita juu ya shaughuli zako.
  • WOGA WAKO.Ninanukuu mwimbaji mmoja hapa, ameimba kuwa woga wako ndiyo umaskini wako.Thubuti leo!
Kwa kuwa na wewe ni mtanzania sasa jaribu kujipima, kwanini huna kitu cha ujasiriamali kwenye ubongo wako?

Naomba uweke nyongeza ya matatizo mengine yenye kuzuia sisi watanzania wajasiriamali tusiweze kukua kiujasiriamali kama wenzetu wa KENYA AU UGANDA.

Nchini Tanzania elimu ya ujasiriamali inahitajika sana ili kuzitumia kwa ufanisi fursa na raslimali zilizopo. Tanzania imejaliwa maziwa, mito, bahari, mabwawa n.k. ambayo siyo kwamba yamejaa samaki tu bali yamejaa pia viumbe wengine kama vile viboko, mamba n.k. Nchi imejaliwa ardhi kubwa ambayo haijatumika, misitu na wanyama mwitu na wale wa kufugwa. Pia nchi imejaliwa kuwa na gesi na madini kama vile almasi, dhahabu, Tanzanite, makaa ya mawe kwa uchache tu. Hata hivyo, vitu vyote hivi havijatumiwa kikamilifu ili kuleta maendeleo ya watu. Kwa maneno mengine, tunakosa maarifa na ujuzi wa kiujasiriamali katika kuzibadilisha fursa hizo kuwa maendeleo. Iwapo tunataka maendeleo endelevu lazima tutengeneze/tuandae watu ambao wanaweza:
•Kuendeleza bidhaa mpya
•Kugundua huduma na njia mpya zinazotilia mkazo matumizi halisi katika kiwanda au shirika
•Kugundua na kutumia masoko mapya ambayo kiwanda au shirika halijayatumia
•Kugundua na kutumia nyenzo mpya za utoaji raslimali ambazo hazijawahi kutumika
•Kuwa tayari kupambana na hatari yoyote kwa faida ya nchi
Nchini Tanzania tunahitaji watu ambao wanaweza kuleta tija katika uzalishaji kwenye taasisi au mashirika. Utafiti uliofanyika hivi karibuni umeonesha kwamba huduma za afya nchini Tanzania ni duni sana. Kwa mfano, asilimia 53 ya wagonjwa wanaofika hospitalini huhudumiwa baada ya kusubiri kwa muda wa masaa mawili au matatu na asilimia 19 ya wagonjwa ambao hufikishwa hospitalini huombwa rushwa. Haya yote hutokea kutokana na kukosekana kwa elimu ya ujasiriamali. Hawaijali raslimali watu na wanadhani kuwa uzalishaji unaweza kupatikana kwa njia ya hongo. Ili kuleta ufanisi na tija katikaupatikanji wa huduma na bidhaa, taasisi au shirika lolote linapaswa kuwajumuisha wajasiriamali ambao wanaweza kuleta tija kwenye huduma na bidhaa kwa lengo la kuongeza uzalishaji.

Hitimisho

Elimu ya ujasiriamali si ya zamani kama zilivyo fani nyingine kama vile sayansi ya siasa, falsafa na sosholojia, lakini ujasiriamali umeleta mabadiliko makubwa tangu kuanza kwake. Kompyuta, mashine za ATM, simu za mikononi, kwa uchache tu ni bidhaa zinazotokana na ujasiriamali. Ijapokuwa mtu anaweza kuwa na sifa za ujasiriamali, ni sharti afundishwe somo hilo ili kumpatia maarifa na ujuzi wa kushindana katika ulimwengu kwa ujumla wake. Ufundishaji makini wa ujasiriamali utawezesha kupatikana kwa maendeleo endelevu na hivyo kuwawezesha watu kuwa na maisha mazuri katika nchi zao.
Reactions:

0 comments:

Post a Comment

    Followers